Tuesday, October 16, 2012

Mgodi wa Chumvi Uvinza Hatarini Kutaifishwa - David Kafulila

0 comments
Mbunge acharuka, ushauri wa Mwanasheria Mkuu wasubiriwa

UUZAJI wa vifaa vya mtambo wa kuzalisha chumvi katika Mgodi wa Chumvi Uvinza mkoani Kigoma umezidi kuzua mvutano, safari hii Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, akijiandaa kuwasilisha hoja binafsi bungeni kutaka mgodi huo uliobinafsishwa, utaifishwe.

Kisa cha wito huo wa kutaifishwa kwa mgodi huo ni tuhuma dhidi ya mwekezaji, Yogesh Maneck, kupitia kampuni yake ya Great Lake Mining, kukiuka masharti ya mkataba wa uwekezaji, akidaiwa kutowekeza Sh. bilioni tatu kama alivyoahidi lakini pia kuuza sehemu ya mitambo nchini Iran, mauzo ambayo ameyathibitisha kupitia kwa Meneja Kazi wa mgodi huo, Bonny Mwaipopo.

Lakini wakati Kafulila ambaye amekuwa ‘akipiga kelele’ bungeni kuhusu uuzaji huo, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, naye anadaiwa kumwandikia barua Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa na nakala ya barua hiyo kutumwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema, akitaka ushauri kuhusu uamuzi wa kutaifisha mgodi huo.


Mwandishi wetu alijaribu kuwasiliana na Waziri Muhongo, Waziri Mgimwa, Waziri wa Viwanda na Biashara Dk. Abdallah Kigoda (ambaye ndiye aliyesimamia ubinafsishaji) na Mwanasheria Mkuu, Werema bila mafanikio, simu zao za mkononi zikiita bila majibu.


Lakini kwa mujibu wa Kafulila ambaye anakiri kuusoma mkataba huo katika ofisi za Bunge chini ya ulinzi mkali, mwekezaji amekiuka masharti ya mkataba ambayo ni pamoja na kutowekeza Sh bilioni tatu kama alivyoahidi, pamoja na kuuza vifaa vya mitambo hiyo nchini Iran.


Madai ya Kafulila

Kafulila ambaye ni Mbunge wa Kigoma Kusini ulipo mgodi huo amemweleza mwandishi wetu kwamba, katika ziara yake na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Steven Masele, walibaini vifaa vya mtambo wa mgodi huo kuuzwa nchini Iran.

Anasema kitendo cha kuuza vifaa vya mtambo huo ni kosa ambalo ni kinyume cha mkataba kati ya mwekezaji na serikali na hatua hiyo inatosha kumchukulia hatua kali mwekezaji huyo ikiwa ni pamoja na kutaifisha mgodi huo kutoka kwake.


“Si tu ameuza vifaa vya mtambo wa mgodi nchini Iran lakini pia hakuwekeza Sh bilioni tatu ili kuendeleza mgodi kama anavyotakiwa na mkataba. Mimi nimesoma mkataba japo chini ya ulinzi kwenye ofisi za Bunge, huyu amekiuka masharti ya mkataba,” alidai Kafulila.


Kwa mujibu wa Kafulila, kama serikali kupitia kwa Waziri wa Nishati na Madini haitachukua hatua za kumdhibiti mwekezaji huo, atawasilisha hoja binafsi bungeni kutaka mgodi huo ubinafsishwe.


“Mimi kama Mbunge wa wananchi wanaopaswa kunufaika na mgodi huo, sioni mantiki ya kuendelea na mwekezaji huyu ambaye ameshindwa kuwekeza na badala yake anaharibu, kwa sasa badala ya kuendeleza mtambo anatumia teknolojia ya jua na kuni kuandaa chumvi. Hii inaweza kufanywa hata na Jeshi letu la Magereza au Jeshi la Kujenga Taifa, ni bora kuwapa hawa,” alisema Kafulila.


Uongozi wa mgodi wazungumza

Mwandishi wetu aliwasiliana na uongozi wa mgodi, baada ya kushindwa kumpata Mwenyekiti wa Bodi, Yogesh Maneck, na kufanikiwa kuzungumza na Meneja wa Kazi katika Mgodi huo, Bonny Mwaipopo.

Katika mazungumzo na mwandishi wetu, Mwaipopo alikiri kuuzwa kwa mtambo huo nchini Iran, lakini akisisitiza kwa kusema; “Haukuuzwa mtambo wote, viliuzwa baadhi ya vifaa vya mtambo, yaani evaporators na viliuzwa kwa shilingi milioni 259 na si bilioni 4.5 kama inavyoelezwa na wanasiasa.”


Alisema haukuwa uamuzi sahihi kujenga mtambo huo ambao uendeshaji wake ni wa gharama kubwa na hasa ikizingatiwa kuwa unaendeshwa kwa kutumia mafuta mazito.

“Uwezo wa mtambo huo katika uzalishaji ni kuzalisha tani 60 kwa mwaka lakini kwa miaka yote sita ya uendeshaji wake mtambo haukuwahi kuzalisha kiwango hicho.

Kulifanyika uamuzi mbaya wa kujenga mtambo huu, fikiria unatumia lita kati ya 28,000 hadi 30,000 kwa siku kwa ajili ya kufanya kazi. Kwanza hayo mafuta kuyafikisha huku Uvinza ni gharama na ni vigumu, lakini pia kuna suala la dawa mbalimbali zinazohitajika kwa ajili ya kusafisha mtambo,’ alisema.


Mtambo huo ambao ulijengwa na kampuni ya IBECO ya Italia, kwa mujibu wa maelezo ya Mwaipopo ni vigumu kuufufua na kwamba badala yake, mwekezaji aliamua kutumia teknlojia ya kuni na jua.


“Tunatumia jua kukausha chumvi lakini tunao mtambo wa kuisaga, kuifisha na kuikausha tena chumvi hiyo,” alisema.


Kafulila alisema Mamkala ya Uhakiki wa Migodi (TMAA) ilifanya ukaguzi wake katika mgodi huo na kubaini kuwa ni kweli vifaa vya mtambo wa kukausha chumvi uliojengwa na Waitaliano, uling’olewa vifaa vyake na kuuzwa nchini Iran.



By: Mwandishi Wetu (Raia Mwema)  


 

Leave a Reply

Followers


 
UVINZA FM COMMUNITY RADIO © 2012 | Designed by Emmanuel Hilonga