SERIKALI mkoani Kigoma imeanza mchakato wa kuifunga kambi pekee ya wakimbizi kutoka nchini Burundi ya Mtabila iliyopo wilayani Kasulu mkoani hapa kufuatia kile serikali inachoeleza kuwa wakimbizi hao kukosa sifa ya kuendelea kuhifadhiwa na kupewa hadhi ya
ukimbizi.
Kaimu Mkuu wa Mkoa Kigoma, Danhi Makanga alisema hayo wakati akiongoza wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoani Kigoma na ile ya Wilaya ya Kasulu kutembelea kambi hiyo kujionea mchakato huo.
Makanga alisema kuwa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa katika kikao chake cha Agosti 29 mwaka huu, kilijiridhisha kuwa wakimbizi hao hawana sababu yoyote ya kuendelea kupewa hifadhi ya ukimbizi kutokana na hali ya amani iliyopo nchini mwao Burundi kwa sasa.
Aliongeza kuwa hata maisha wanayoishi sasa kambini hapo yanathibitisha kwamba hawana shida yoyote ya kupewa hifadhi hiyo na kwamba wanatumia nafasi hiyo katika kufanya
shughuli nyingine nje ya hadhi yao ya ukimbizi.
Mkuu huyo wa Mkoa alisema kuwa hivi sasa sehemu kubwa ya wakimbizi hao licha ya
kupata msaada wa chakula bure na mahitaji mengine ya kibinaadamu lakini pia wamejiingiza kwenye kilimo katika vijiji kuzunguka kambi hiyo, kufungua maduka makubwa ya kuuza bidhaa mbalimbali na wengi wao wanamiliki pikipiki na magari ambavyo hutumika
kusafirisha watu kuingia na kutoka kambini humo wakati mwingine isivyo halali.
Kufuatia Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa kujiridhisha na hali hiyo kuanzia juzi askari Polisi wa kikosi maalumu zaidi ya 100 wameizingira kambi hiyo kuzuia wakimbizi kuingia au kutoka ndani ya kambi hiyo ili kuruhusu uhakiki wa idadi halisi ya wakimbizi waliopo kambini humo kufanyika.
Aidha kufuatia kuzingirwa kwa kambi hiyo, juzi wakimbizi zaidi ya 150 ambao walikamatwa nje ya kambi hiyo wakiwa hawana vibali vya kuwaruhusu kutoka nje ya kambi walifunguliwa mashitaka ya kuishi nchini isivyo halali.
Makanga alisema kuwa uongozi wa serikali mkoani humo umejiwekea mkakati wa utekelezaji wa kuhakikisha kwamba kambi hiyo ambayo imebaki kwa sasa ikihifadhi wakimbizi pekee
kutoka nchini Burundi inafungwa hadi kufikia Desemba 31 mwaka huu.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Fraiser Kashai alisema uchunguzi umebaini wengi wa wakimbizi kambini humo ni vijana ambao wamekuwa wakikamatwa katika matukio ya ujambazi wa kutumia silaha.
Naye Mkuu wa Makazi wa Wizara ya Mambo ya Ndani katika kambi hiyo, Frederick Nisajile ameitaka serikali uyagawa maeneo ambayo hapo awali yalikuwa sehemu ya kambi ya wakimbizi ya Mtabila ambayo ni rasilimali muhimu kwa kilimo.
Nisajile alisema kuwa baada ya kufungwa kwa Mtabila Moja na Muyowosi maeneo hayo yamebaki bila kutumiwa na wakimbizi licha kuyatumia kwa kilimo, lakini pia huyatumia kama maeneo ya kujihifadhi kwa ajili ya kufanya vitendo vya kihalifu.