Tuesday, October 16, 2012

Asha Baraka aweka wazi ukweli kuhusu kuzirai kwake

0 comments
UTANGULIZI
 
Iliripotiwa kupitia vyombo vingi vya habari kuwa nilianguka ghafla na kupoteza fahamu nilipokuwa nikishiriki katika uchaguzi wa C.C.M katika ngazi ya Wilaya mpya ya Uvinza Mkoani Kigoma.
Mara baada ya kutangazwa kwa habari zile, ziliniletea usumbufu mkubwa kwangu mimi mwenyewe pamoja na ndugu zangu wa karibu kwa kupokea simu mara kwa mara zilizokuwa zikitaka kujua ukweli wa taarifa.

UKWELI ULIVYO.
 
Nilichukua fomu kwa ajili ya kugombea Ujumbe wa NEC ya C.CM kupitia Wilaya mpya ya Uvinza iliyoko Mkoani Kigoma. Mara baada ya kipindi cha Kampeni kumalizika, ilifika wakati wa uchaguzi ambao ulifanyika siku ya Jumapili tarehe 30-09-2012.

Mara baada ya kumalizika kwa taratibu zote za uchaguzi ulifika wakati wa kupokea matokeo, wakati taratibu za upokeaji matokeo zikiendelea, nilianza kuhisi dalili ya PUMU (ATHMA) kunizidia kutokana na kukosa hewa kulikosababishwa na udogo wa chumba kilichokuwa kikitumika kwa ajili ya shughuli hiyo, nilimuomba Msimamizi wa Uchaguzi ruhusa ya kutoka nje ili nipate nafasi ya kupata hewa nzuri lakini Msimamizi wa Uchaguzi kwa vigezo vya taratibu za uchaguzi wa C.C.M na kutokujua kama ni mwenye matatizo ya PUMU alinikatalia kutoka nje ya chumba.

Mara baada ya kukataliwa nilitii maamuzi ya msimamizi na kuendelea kuivumilia hali ile mpaka ilipokuwa mbaya kabisa nilimuomba tena msimamizi ili nitoke nje na alinikubalia.
nilipotoka nje nilijilaza chini kwa kukosa nguvu na kwa kuwa nje palikuwa na watu wengi walidhani nimezidiwa basi kila mtu alianza kutaka kunipa huduma ya kwanza wapo walionivua viatu, wapo walionimwagia maji na wapo pia waliokuwa wakinipepea.
nilipoona hali ya taharuki imezidi ndipo nilipomuomba Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya ya Uvinza Mhe. Fatuma Nyembo usafiri ili nikachome sindano ya kutuliza PUMU ambayo ilianza kunizidia.

Mara baada ya kuchoma sindano nilirejea katika hali yangu ya kawaida kama hapo awali. Ikumbukwe maradhi ya PUMU yamekuwa yakiniandama kwa muda mrefu sasa takribani kwa miaka 13. Mara zote huwa inanizidia lakini nimekuwa nikichoma sindano na kurejea katika hali yangu ya kawaida.

Pia hali ya pumu kunizidia ilikuwa ni mara baada ya shuguli nyingi za kichaguzi za ndani ya C.C.M kumalizika na kuibuka mshindi wa kwanza kwa kujizolea kura 322 huku nikimwacha mbali mpinzani wangu JOSEPHINE NAWEZA aliyepata kura 210.

Kutokana na ushindi huo mimi sasa hivi ni mjumbe wa NEC kupitia wilaya ya Uvinza yenye tarafa za Nguruka, Uvinza, Malagarasi, Sunuka, Kazuramimba, Kandaga, Ilagara, Igalula, Sigunga, Bihungi, Kalya, Mtego wa Mti, Mganza na Itebula.

MWISHO NA HITIMISHO.
 
Napenda kutoa ahsante kwa wale wote walioguswa na mpaka kunitafuta kwa njia moja au nyingine kutokana na habari hii na kuwajulisha kuwa mimi nipo imara kabisa na ninaendelea na shughuli zangu kama kawaida na kwa sasa nipo bado Kigoma.

AHSANTENI
ASHA BARAKA (MNEC)
MKURUGENZI WA ASET

Leave a Reply

Followers


 
UVINZA FM COMMUNITY RADIO © 2012 | Designed by Emmanuel Hilonga